Tuesday 30 September 2014

MAGONJWA YA MENO NA FIZI



Magonjwa ya fizi na meno


Magonjwa ya fizi na meno ni chanzo kikuu cha kupoteza meno kwa watu wenye umri mkubwa/watu wazima, na pia magonjwa haya huhusishwa na magonjwa ya moyo na kiharusi (stroke).

Ikiwa magonjwa haya ya fizi yatatambuliwa mapema (gingivitis), yanatibika vizuri na kuepusha madhara zaidi.
Ikiwa tatizo hili halitopata tiba mapema, ugonjwa hukomaa zaidi (periodontitis) ambapo mfupa unaoshikilia jino/meno hushambuliwa na kuharibiwa.

Kusafisha meno kwa kupiga mswaki mara mbili kwa siku, matumizi ya nyuzi-safishi (dental floss), kumwona daktari wa meno kwa uchunguzi mara kwa mara na kusafisha meno kitaalamu kwa utabibu wa meno, kutasaidia kuepuka madhara ya magonjwa ya fizi.

Uchunguzi wa kinywa na kusafisha meno kitaalamu
Ni wangapi kati yetu wenye desturi ya kumwona daktari wa meno walau mara mbili kwa mwaka (walau kila baada ya miezi sita)? Mara nyingi wengi wetu huhangaika na foleni za kumwona daktari wa meno pale tu tunaposumbuliwa na maumivu ama ya jino ama kidonda kinywani ama kwa sababu ya hali zinginezo zinazotulazimisha kumwona daktari wa meno.

Kusubiri mpaka tusukumwe na maumivu ya meno/kidonda kinywani ama ajali yoyote kunatunyima fursa bora zaidi ya kuchunguzwa afya ya kinywa na meno na kusafishwa meno ili kuepusha madhara ya magonjwa ya kinywa na meno kabla hayajatokea ama kukomaa.

Kupiga mswaki mara mbili kwa siku
Kupiga mswaki kwa ufanisi walau mara mbili kwa siku huondoa ukoko unaogandamana kinywani na kusababisha kuoza kwa meno. Ukoko huu ni ute laini unaoganda kwenye sehemu mbalimbali za jino/meno huku ukiwa na mamilioni ya vimelea vya magonjwa (bakteria).

Matumizi ya nyuzi-safishi (dental floss) kila siku husaidia kuondosha ukoko maeneo ambako mswaki haufiki, vile vile kuondosha ukoko huu kunasaidia kujikinga na magonjwa ya fizi.

Sababu za harufu mbaya mdomoni
Takriban asilimia 85 ya watu wenye harufu mbaya kinywani huwa na magonjwa ya kinywa na meno, ikiwa harufu mbaya kinywani inasababishwa na magonjwa kinywani, dawa za kusafisha kinywa (mouthwash) haziwezi kuondoa tatizo zaidi ya kulifunika kwa muda tu.

Hakuna sababu ya kuona haya kumwambia daktari wa meno kuhusu harufu mbaya kinywani inayokusumbua, kwa vile kumwambia na kujadili tatizo lako ni njia ya kuelekea kwenye tiba ya uhakika. Matumizi ya nyuzi-safishi (dental floss) kila siku, kusafisha meno na ulimi kwa mswaki walau mara mbili kwa siku yaweza kuondoa harufu mbaya kinywani kwa kiasi kikubwa.

Chakula bora na umuhimu wake kwa kinywa na meno
Ulaji wa vyakula na vinywaji vyenye sukari na visivyo na virutubisho vya mwili vinapochanganyikana na vimelea vya magonjwa (bakteria) hutengeneza tindikali ambayo hushambulia ukuta wa nje wa jino (dental enamel). Kushambuliwa kwa enameli na tindikali husababisha mashimo kwenye meno na magonjwa ya fizi.


No comments:

Post a Comment